Allahu taala kutokana na huruma zake kwa watu wote hapa duniani, basi amewaumbia na kuwashushia vitu vyenye faida..Wale waumini ambao watatubia wakiwa bado wako duniani,basi hata kama
dhambi zao zitakuwa ni za ukubwa gani, hawa wafikapo akhera kwa uhakika kabisa dhambi zao watasamehewa. Wale ambao wamekufa bila ya kuleta toba na ikathibiti kwao kuingia motoni miongoni mwa waumini, basi wale awatakao atawasamehe na kuwaingiza peponi. Niyeye pekee aliyeumba kila chenye roho na kukifanya kiendelee kuwepo kila muda, pamoja na kuvilinda vyote na madhara na vitisho. Nami ninaanza kuandika kitabu hiki kwa kujikinga kwa jina tukufu la Allah mwenye sifa hizo tulizozitaja.
Shukrani zote zinamstahikia Allahu taala. Swala na salamu ziwe juu ya Mtume wa Allah. Dua zenye kheri ziwe juu ya watu wa nyumbani kwake walio wasafi na masahaba wake, radhi za Allah ziwe juu yao walio waadilifu na wakweli.